Ghana yatuma satelite yake ya kwanza anga za juu
Ni mara chache sana kusikia mambo makubwa ya kisayansi yakitokea katika nchi za Afrika, lakini hilo litabadilika muda kadri unavyozidi kwenda mbele.
Ghana imefanikiwa kutuma satelaiti yake ya kwanza kabisa katika anga za juu.
GhanaSat-1, ambayo iliundwa na wanafunzi katika Chuo Kikuu cha All Nations cha Koforidua, ilitumwa hadi kwenye mzingo wa dunia kutoka kwenye Kituo cha Kimataifa cha Anga za Juu.
Shangwe, vifijo na nderemo vilitanda hewani baada ya ufanisi huo miongoni mwa watu 400, wakiwemo wahandisi, waliokuwa wamekusanyika katika mji huo wa kusini mwa Ghana kutazama moja kwa moja picha za uzinduzi huo wa satelaiti hiyo.
Mawasiliano ya kwanza kutoka kwenye satelaiti hiyo yalipokelewa muda mfupi baadaye.
Kurushwa angani kwa satelaiti hiyo ni kilele cha mpango wa miaka miwili, uliogharimu jumla ya $50,000 (£40,000).
Chuo kikuu hicho kilipokea usaidizi kutoka kwa Shirika la Upelelezi wa Anga za Juu la Japan (JAXA).
Satelaiti hiyo itatumiwa kufuatilia pwani ya Ghana kwa ajili ya kuunda ramani ya kina ya pwani ya taifa hilo pamoja na kufuatilia yanayojiri.
Kadhalika, itatumiwa kuongeza uwezo wa taifa hilo katika sayansi na teknolojia ya anga za juu.
Mratibu wa mradi huo Dkt Richard Damoah anasema kufanikiwa kwa mradi huo ni kama mwanzo mpya kwa taifa hilo.
"Hilo limetufungulia mlango kwetu kufanya mambo mengi zaidi kutoka anga za juu," ameambia BBC.
Amesema mradi huo "utatusaidia kutoa mafunzo kwa vizazi vijavyo jinsi ya kutumia satelaiti katika shughuli mbalimbali katika kanda yetu.
"Kwa mfano, [kufuatilia] uchimbaji madini haramu ni moja ya mambo ambayo tunakusudia tutafanikiwa kufanya (kwa kutumia satelaiti hiyo)".
Source: BBC
No comments